Swahili   |   English
Kuhusu Wosia

RITA kama Wakala wa Serikali ina wajibu wa kulinda haki za kimsingi ambapo imeanzisha kitengo cha kuandika na kutunza Wosia.Hii ni kutokana na matatizo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii baada ya mhusika kufariki,na kutokana na unyanganyi wa mali wakati mmoja wa wanafamilia anapofariki.
Wakala una dhamana ya kusimamia mirathi na uzoefu wetu wa muda mrefu unaonyesha kwamba mtu anapofariki bila ya kuacha wosia kunatokea migogoro, kama vile:

  • Familia kunyang’anywa mali.
  • Mafarakano baina ya wana familia.
  • Kesi za mirathi zinapofunguliwa huchukua muda mrefu kuisha.
  • Mgogoro wa mahali pa kumzika marehemu.

SABABU ZA RITA KUANZISHA KITENGO CHA WOSIA

  • RITA ni chombo cha serikali chenye dhamana ya kusimamia mirathi.
  • Utunzaji wa wosia ni moja ya kazi zilizoainishwa kwenye sheria iliyoanzisha Wakala (Executive Agency Act, Cap 30 1997 .Chini ya Tangazo la Serikali Na. 397 /2005).
  • RITA kama wasimamizi wa mirathi wenye ujuzi na  uzoefu  wa muda mrefu, Uzoefu unaonyesha kwamba  inakuwa vigumu kutekeleza majukumu ya usimamizi wa mirathi pasipo kuwa na wosia.
  • RITA inatoa huduma nzuri, kwa urahisi na gharama nafuu,ambayo kila mwananchi ataweza kuimudu.
  • RITA ina Ofisi katika wilaya zote Tanzania bara hivyo itakuwa rahisi kuwafikia wananchi wengi na kufaidika na huduma hii.

Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia Wajane na Watoto wa marehemu wakipoteza haki zao kwa waume kufa bila kuacha Wosia.Hata wale ambao wametayarisha wosia wanakuwa hawahifadhi mahali salama matokeo yake ni kupoteza haki na malengo husika.
Pia wananchi wengi hawafahamu sehemu za kutunza Wosia  kama Mahakama Kuu au Benki. Hata wachache wanaozifahamu wanashindwa kufanya hivyo kutokana na gharama za kutunzia wosia  kuwa kubwa.
RITA kama msimamizi wa haki za urithi na nyinginezo inao wajibu kuona kwamba haki za Urithi zinalindwa kwa misingi hiyo imeanzisha kitengo cha Wosia ambacho kitashughulika na kuandika na kutunza Wosia kwa huduma nzuri,usiri na gharama nafuu ambayo kila mwananchi ataweza kumudu.

WOSIA
MAANA YA WOSIA

Ni tamko au maandishi anayotoa mtu wakati wa uhai wake akielezea mazishi yake yatakavyofanyika likionyesha mahali atakapozikwa au jinsi mali zake zitakavyogawiwa kwa warithi wake baada ya kifo chake.

AINA ZA WOSIA
Kuna aina mbili za Wosia;

  • Wosia wa maandishi
  • Wosia wa mdomo/matamshi