Ujumbe kutoka Nchini Lesotho ukiongozwa na  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Ndani wa Nchi hiyo Bw. Nkhotha Machachamise pamoja na Mkurugenzi wa Ulinzi wa haki za Sheria kutoka RITA Bw. Francis Kugesha wametembelea vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya uzazi, baba, mama  na mtoto kujifunza namna huduma ya usajili wa vizazi na vifo  zinavyofanyika.
Lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano kati ya nchi Tanzania na Lesotho Pamoja na kujifunza mifumo ya usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu  na Takwimu ambayo katika ukanda huu wa Afrika imeonesha tumefanya vizuri.
Ujumbe wa wataalamu hao, umefika kwenye Hospitali ya Wilaya Kivule na Kituo cha Afya Pugu kujionea zoezi la usajili na ugawaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa Watoto wanaozaliwa katika vituo hivyo.
Akizungumza kuhusu walichojionea, Bw. Machachamise amewapongeza wasajili wasaidizi wanaofanya kazi kwenye vituo hivyo na kusifu namna Serikali ya Tanzania kupitia taasisi yake ya RITA ilivyofanikisha kupeleka mifumo kwenye hospitali ambapo watoto wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kwa muda mfupi mara baada ya kuzaliwa.
‘’Tumejifunza mifumo na utaratibu mzuri wa utoaji wa huduma kwa wananchi, tunafahamu Tanzania ni nchi kubwa, ina watu wengi ukilinganisha na Lesotho yenye watu milioni mbili na nusu lakini mmeweza kuweka mifumo iliyowezesha kuwafikia watu wote katika maeneo yote ya nchi, kwa kweli hongereni sana’’. Alisema Machachamise.
Ziara hiyo ni moja ya ziara nyingi zinazofanywa na mataifa mbalimbali barani Afrika  kuja Tanzania kujifunza usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu ambapo kwa Tanzania imepiga hatua nzuri kwenye mifumo ya usajili na kusaidia katika mipango mbalimbali ya maendeleo.
Tags : #RITA