Deprecated: explode(): Passing null to parameter #2 ($string) of type string is deprecated in /data/ritago/public_html/news.php on line 40
VYETI VYA KUZALIWA SASA KUTOLEWA NDANI YA SAA 48
RITA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
MEDIA CENTRE
December
12
2025
VYETI VYA KUZALIWA SASA KUTOLEWA NDANI YA SAA 48
- - -
`

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amezindua mpango mpya wa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa ndani ya saa 48 za kazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya mfumo wa eRITA, ikiwa ni jitihada za serikali kuhakikisha huduma zote muhimu ja jamii zinawafikia wananchi kule walipo ili kurahisisha upatikanaji wake.

Uzinduzi wa mpango huo umefanyika leo Disemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo Dkt. Homera ameitaka RITA kusimamia na kutekeleza mpango huo kwa weledi wa hali ya juu huku akibainisha uzoefu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuwa unatosha kufanikisha azma hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Homera amesema kuwa, mpango huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza kuwa taasisi zote za umma zitoe huduma kidijitali na kuifanya mifumo hiyo kuwasiliana na hivyo kwa upande wa RITA tayari imeanza kutoa huduma ya vyeti vya kuzaliwa ndani ya saa 48 za kazi kupitia mfumo wa eRITA.

“Mfumo huu tuliouzindua hii leo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kuhakikisha vyeti vya kuzaliwa vinapatikana kwa wakati, ili wananchi wapate huduma nyingine muhimu zinazotegemea cheti hicho kama vile elimu, bima ya afya, hati za kusafiria kule uhamiaji, vitambulisho vya Taifa na haki nyingine hasa usimamizi na ufunguaji wa mirathi kule mahakamani.” alisema Dkt. Homera.

Aidha, Waziri Mhe. Dkt Homera aliipongeza RITA kwa mafanikio makubwa waliyoyapata katika utoaji wa huduma ambapo hadi kufikia Novemba 25 mwaka huu, wakala huo umefanikiwa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa milioni 11.5.

‘‘Kwa mujibu wa takwimu za RITA, jumla ya Watanzania milioni 20 wamefanikiwa kusajiliwa hadi Novemba 2025, ikilinganishwa na Watanzania 205,000 pekee waliokuwa wamesajiliwa mwaka 2004, hii ni hatua kubwa kwa RITA na nawaagiza waongeze kasi na uratibu mzuri Zaidi ili wananchi wote wenye sifa wasajiliwe na kupatiwa huduma hiyo’’. Alisema Dkt. Homera.

Wakati huo huo, Mhe. Waziri Homera aliitaka RITA kuendelea kusimamia kwa ufanisi taasisi zote zilizo chini yake pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya uandishi wa wosia na usimamizi wa mirathi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima katika jamii.

Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi alisema mahitaji ya vyeti vya kuzaliwa ni makubwa na kwamba mpango huo mpya utasaidia kupunguza msongamano wa wananchi wanaosubiri huduma katika taasisi mbalimbali za umma.

 

“RITA ndiyo taasisi ya kwanza kutoa utambulisho rasmi wa Mtanzania pale tu anapozaliwa na cheti hiyo ni muhimu sana katika upatikanaji wa huduma nyingine kutoka mbalimbali hapa nchini ikiwemo upatikakanaji wa hati ya kusafiria na mengineyo,” amesema Bw. Kanyusi.

Akielezea mafanikio mengine ya RITA, Bw. Kanyusi amesema kuwa hadi Novemba 25 mwaka huu, RITA imefanikiwa kufanya usajili na kutoa  vyeti vya ndoa zaidi ya milioni moja, vyeti vya vifo zaidi ya elfu 12, pamoja na maboresho mbalimbali ya kiutawala na TEHAMA ikilenga mifumo ya kidijitali na vitendea kazi.

Wakati hayo yakijiri, Mmoja wa wananchi aliyenufaika na mpango huo, Bi. Fatuma Saidi, alisema alipata cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake ndani ya saa 48 za kazi, jambo ambalo halikulitarajia kutokana nah apo awali kushindwa kufanya hivyo kutokana na kutofahamu taratibu za kuomba huduma hiyo kwa njia ya mtandao.

Hapo mwanzo mume wangu aliniambia kuwa  kupata cheti cha kuzaliwa nitasubiri kwa wiki mbili au tatu, lakini nilishangaa kuambiwa ndani ya saa 48 kuwa cheti changu kiko tayari,” alisema Bi. Fatuma.