Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amewataka wajumbe wa Bodi za Wadhamini nchini kuzingatia Sheria, kanuni na katiba zao wakati wa kutekeleza majukumu yao ili kulinda haki na kusimamila rasilimali za taasisi zao kwa maslahi mapana ya jamii husika.
Mhe. Dkt. Homera ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Wajumbe wa Bodi za Wadhamini wa mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida, Iringa na Manyara kilichofanyika leo Novemba 27, 2025 mkoani Dodoma.
Pia, Mhe. Dkt. Homera ameiagiza RITA kuboresha mfumo wake wa kidijitali wa usajili wa Bodi za Wadhamini, kufanya mapitio ya Sheria ili ziendane na uhitaji wa sasa, kuongeza wigo wa kliniki za utoaji wa huduma ili kuwafikia wananchi huko walipo pamoja na kutoa mafunzo na usimamizi wa karibu ili kutatua changamoto za kiutendaji za bodi hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya RITA Dkt. Amina Msengwa amesema kuwa, matumizi ya mfumo wa kidijitali wa eRITA umewezesha kuongezeka kwa usajili wa Bodi mpya za Wadhamini, ufuatiliaji wa taarifa na kurahisisha upatikanaji wa takwimu kwa wakati.
Naye Kabidhi Wasii Mkuu Bw. Frank Kanyusi amesema kwa sasa RITA wamejipanga kuhakikisha taasisi zote, vyama vya siasa, vilabu vya vichezo na asasi za kiraia zinasajili na kufanya mabadiliko ya wajumbe wa bodi za wadhamini kwa wakati kulingana na Sheria na katiba zao ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara inayosababishwa na baadhi wa wajumbe kung'ang'ania nafasi hizo.
Bw. Frank Kanyusi amesema, Wakala imeongeza wigo wa huduma tembezi yaani Mobile Clinics nchi nzima panoja na kuimarisha elimu kwa umma kupitia vyombo ya habari.
Pia, amebainisha kwamba, hadi sasa RITA imesajili jumla ya bodi za Wadhamini zipatqzo 5,211, zikiwemo bodi 2,876 za taasisi za kijamii, 2,161 za taasisi za kidini, 19 za vyama vya siasa, 24 za vyama vya michezo na 150 za kifamilia.
Amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Suraya 318, RITA ina jukumu kusimamia usajili na utendaji wa bodi hizo, huku akiweka wazi changamoto za baadhi ya bodi hizo zikiwemo usimamizi hafifu wa mali, uelewa mdogo wa sheria, mabadiliko yasiyo ya kikatiba ya uongozi, migogoro ya mara kwa mara pamoja na ubadhilifu wa mali na matumizi mabaya ya feza za taasisi zao.