RITA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
MEDIA CENTRE
August
10
2026
MAADHIMISHO YA SIKU YA USAJILI WA MATUKIO MUHIMU YA BINADAMU NA TAKWIMU BARANI AFRIKA (CRVS DAY 2026)
News & Update
`

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye mifumo ya kidigitali, kuhamasisha wananchi, na kuhakikisha kuwa huduma ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu (vizazi, vifo, ndoa, talaka na watoto wa kuasili) inamfikia kila mtu bila kujali anaishi wapi au ana hali gani ya kiuchumi ili kwenda sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameyasema hayo Agosti 10, 2026  wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika, (CRVs Day 2026), yaliyofanyika kitaifa katika viwanja Nanenane vya Dkt. John Samwel Malecela Mkoani Dodoma.

"Siku hii ni fursa ya kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kusajili matukio kama haya ya vizazi, vifo, ndoa, talaka na mengine mnuhimu yanayotokea kila siku katika maisha ya binadamu." amesema Dkt. Homera

Aidha alisisitiza kuwa Usajili wa matukio mubhimu ni urithi wa kitaifa, ni alama ya heshima kwa kila mwananchi na ni injini ya maendeleo ya taifa.

Dkt, Homera, amesema kwa mujibu wa takwimu za RITA, kufikia mwezi Juni 2026. Usajili wa vizazi kwa Watoto umeongezeka kutoka asilimia 55% mwaka 2020 hadi asilimia 68%mwaka 2025, ikiwa na lengo la kufikia asilimia 100% ifikapo 2030.

Pia, ameongeza kuwa, katika kuhakikisha tunafikia mipango ya maendeleo na kuendana na Dunia ya leo inayo endeshwa na teknolojia, ni vyema wadau wote kuuanganisha nguvu katika kuimarisha Usajili wa matukio muhimu kwa njia ya kidigitali.

Kwa upande wake Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi, amesema Maadhimisho hayo yameanzishwa kwa lengo la kuongeza mwamko na kasi ya wananchi kusajili matukio ya Vizazi, Vifo, Ndoa,Talaka na Kuasili Watoto mara tu yanapotokea.

"Katika kuadhimisha siku hii, Wakala imefanikisha kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 161 wenye uhitaji maalum kutoka katika  Makao ya Taifa ya Watoto ya Kikombo mkoani Dodoma, pamoja na watoto 320 kutoka Kata ya Mtwango wilayani Mufindi mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya kujali na kurejesha kwa jamii hasa makundi ya wananchi wenye mahitaji maalum". Amesema Bw. Kanyusi.