Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera ameridhishwa na utekelezaji wa huduma ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa njia ya kidijitali kupitia eRITA ndani ya saa 48, huku akiwataka watumishi wa RITA kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili wananchi waendelee kupata huduma bora na kwa wakati.
Amezungumza hayo katika ufunguzi wa Kliniki ya Huduma za Msaada wa Kisheria uliofanyika leo Januari 05, 2026 katika viwanja vya stendi ya zamani mkoani Morogoro.
Mhe. Homera ameongozana na viongozi mbali mbali akiwemo Mkuu wa mkoa wa Morogoro Adam Malima na Naibu kabidhi wasii mkuu Bi. Irene Lesulie, walipofika katika banda la Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) na kuona huduma mbali mbali zinazotolewa na Wakala.
Sambamba na hilo, Mhe. Homera alikabidhi hadharani vyeti vya kuzaliwa kwa baadhi ya wananchi mkoani humo, walionufaika na huduma hiyo ya upatikanaji wa vyeti ndani ya saa 48.
Kliniki hiyo ya siku mbili inahusisha wadau mbali mbali na sisi kama Wakala tupo kutoa huduma na elimu kwa wananchi wa mkoa wa Morogogoro, hivyo tunawahimiza wajitokeze kwa wingi kupata msaada na huduma.