Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ametembelea kuona huduma zitolewazo na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa wananchi kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea katika Mkoa wa Shinyanga.
Katika ziara yale leo Mei 19, 2026, Mhe. Mhita ameongozana na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro pamoja na kamati ya ulinzi ya mkoa. Viongozi hao walipata fursa ya kushuhudia namna wananchi wanavyopatiwa huduma, hususani usajili wa vizazi na vifo, pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa kuwa na nyaraka hizo katika kupata huduma za kijamii.
Aidha, Mhe. Mhita alipokea taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa huduma zinazotolewa na RITA tangu kuanza kwa kampeni hiyo. Taarifa hiyo imebainisha kuwa jumla ya wananchi 5,459 wamefikiwa na kupatiwa huduma za usajili pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa nyaraka za utambulisho wa kisheria. Takwimu hizi zinaonesha mwitikio mkubwa wa wananchi na mafanikio ya kampeni katika kuwafikia watu wengi wenye uhitaji.
Akizungumza machache katika ziara yake, Mhe. Mhita alieleza kuridhishwa na kazi inayofanywa na RITA pamoja na taasisi nyingine zinazoshiriki katika kampeni hiyo katika kuunga mkono juhudi za Serikali. Alisema huduma zinazotolewa zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kuwa zinawawezesha kupata nyaraka muhimu za utambulisho wa kisheria na kuongeza uelewa kuhusu haki zao za msingi hivyo kuwaasa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kujitokeza kwa wingi kutumia fursa ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ili kupata huduma mbalimbali zinazotolewa, kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anatambuliwa kisheria na anapata haki zake stahiki.