Kufuatia mwendelezo wa mpango wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia kampeni mbalimbali za usajili wa vyeti vya kuzaliwa zinazoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, kumekuwa na muitikio mkubwa kutoka kwa wananchi.
Katika Kata ya Mbagala, Viwanja vya Zakhem, ambako RITA imeweka kambi maalum kwa ajili ya kutoa huduma za usajili kuanzia tarehe 17 hadi 26 Agosti, 2026, wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa hiyo kupata huduma kwa urahisi na kwa wakati.
Kupitia kampeni hiyo ya siku 10, wananchi wanapata fursa ya kukamilisha taratibu za usajili na kupatiwa vyeti vyao vya kuzaliwa papo hapo baada ya kukamilisha taratibu husika. Huduma hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi, kwa kuwa cheti cha kuzaliwa ni nyaraka muhimu ya utambulisho inayowezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali zinazohitaji uthibitisho wa taarifa za kuzaliwa.
Muitikio huo unaendelea kuonesha umuhimu wa kusogeza huduma karibu na wananchi, huku RITA ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kupunguza usumbufu, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata nyaraka muhimu za utambulisho kwa wakati.